Spika wa bunge la Marekani, Nancy Pelosi, amemuidhinisha Joe Biden kuwania urais nchini humo na hivyo kuwa miongoni mwa vigogo wa chama cha Democrat, ambao wametangaza kumuunga mkono makamu huyo wa zamani wa rais.

Hatua hiyo ya Pelosi inafuatia ile ya rais wa zamani Barack Obama, makamu wa zamani wa rais Al Gore, pamoja na maseneta Bernie Sanders na Elizabeth Warren, waliomuidhinisha Biden mapema mwezi huu.

Kupitia ujumbe uliotolewa leo kwa njia ya video, Pelosi ametaja uzoefu wa Biden katika serikali ikiwemo wajibu wake katika kupitisha sheria ya bima nafuu ya afya kama ushahidi wa sifa zake za uongozi.

Amesema Biden yuko katika nafasi nzuri ya kuiongoza nchi hiyo inayokumbwa pia na janga la corona.

Uidhinisho wa Pelosi umejiri wakati unaofaa kwa Biden, ambaye amekuwa mbioni kuendeleza hadhi ya juu katika kipindi hiki cha janga la corona katika kinyang’anyiro cha kuwania urais.

Wademocrat, wanatumai kujenga umoja kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Novemba 3 dhidi ya Rais Donald Trump.