Jumatano wiki hii imetimu wiki moja toka Tanzania kutoa takwimu za mwisho za ugonjwa wa virusi vya corona nchini humo.
Hali hiyo inatokea wakati serikali ya nchi hiyo ikiwa inakosolewa juu ya namna inavyolishughulikia janga la corona.
Usiri wa taarifa ni moja ya maeneo ambayo wapinzani na wanaharakati wa ndani na nje ya nchi hiyo wamekuwa wakilalamikia.
Mpaka sasa taarifa rasmi ni kuwa, nchi hiyo imethibitisha wagonjwa 480 na vifo 10, pamoja na watu 167 kupona.
Ni dhahiri kuwa katika kipindi cha wiki moja iliyopita kuna mabadiliko kwenye takwimu hizo, japo hayajawekwa wazi na serikali.
Pia, hakuna takwimu mpya, mambo kadhaa kuhusu mwenendo wa korona yametokea nchini humo katika kipindi hicho cha wiki moja na haya ni baadhi:
Je, serikali imesema nini kuhusu tuhuma za usiri?
Alhamisi ya wiki iliyopita, yaani siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Tanzania kutoa takwimu mpya, Waziri wa Afya wa nchi hiyo alikanusha bungeni kuwa serikali inafanya usiri katika kutoa takwimu.
"Waziri Mkuu kaongea jana, mimi naongea…mwanzoni (mlikuwa mnasema) kwanza watu wenyewe wachache. Sasa tumetoa (mnasema) tumeshinda nchi zote za Afrika Mashariki. Hivi tungekuwa tunaficha tungetoa takwimu hizi ambazo tunaonesha Tanzania tuna wagonjwa wengi kuliko nchi nyengine za Afrika Mashariki. Tusingetoa hizo takwimu. Kwa hiyo hakuna usiri, tunazitoa kadri tunavyozipata kutoka maabara," alisema Waziri Mwalimu.
Bi Mwalimu hata hivyo aliliambia bunge kuwa hakukuwa na ulazima wa kutoa taarifa kila siku.
"Wataalamu wameniambia, 'Waziri huna haja ya kutoa takwimu kila siku. Sharti la kwanza la WHO (Shirika la Afya Duniani) lilikuwa ni kutoa taarifa ya kwanza ya kwamba tumepata case (mgonjwa) ya kwanza Covid-19 Tanzania', na taarifa hiyo tumetoa."
Wakati akizungumza bungeni Tanzania ilikuwa juu ya Kenya kitakwimu, lakini kutokana na ukimya wa wiki moja, huku Kenya ikiendelea kuripoti takwimu mpya, kwa sasa Kenya imethibitisha wagonjwa 580.