Ni rasmi sasa, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Bernard Membe amejiunga na chama cha upinzani ACT- Wazalendo.

Uanachama wake mpya katika ACT- Wazalendo umetangazwa leo na kiongozi wa chama hicho Zitto Kabwe katika mkutano wa wanahabari wadau wengine kutoka ulimwenguni kote uliofanyika katika mtandao wa Zoom.

Membe amesema amejiunga kama mwanachama wa kawaida lakini yuko tayari kutumikia chama hicho kwa ngazi na namna yoyote ile.

"Kilichonivutia katika chama cha ACT-Wazalendo ni katiba ya chama hicho na itikadi yake ya kutaka kuleta mabadiliko," amesema Membe

Aidha bwana Zitto Kabwe amemtia moyo Membe kuchukua fomu kuwania nafasi ya uongozi.

Membe aliitikia kwa kuahidi kwamba atakuwa tayari kushiriki katika kinyang'anyiro cha uchaguzi.

"Watanzania watafurahia uchaguzi huu ujao," ameahidi Membe.

Kuhusu vyama vya upinzani kuungana na kuweka mgombea urais mmoja, Kabwe alisema mazungumzo baina ya vyama bado yanaendelea.

Zitto Kabwe
Maelezo ya picha,

Zitto Kabwe, mwenyekiti wa chama cha upinzani Tanzania ACT-Wazalendo

Awali Kabwe alielezea mazingira ya uchaguzi ujao kuwa hayatapelekea uchaguzi ulio huru na wa haki akitaja pamoja na mambo mengine kutoamini uhuru wa tume ya uchaguzi na weledi wa jeshi la polisi.

BBC ilipomuuliza kwa nini bado wataendelea na uchaguzi ilihali hawaamini mazingira kupelekea uchaguzi huru na wa haki Kabwe alisema kutokushiriki pia uchaguzi si jawabu la changamoto kwa demokrasia Tanzania.

"Tumeona katika uchaguzi uliopita visiwani Zanzibar na mahali pengine duniani ambapo vyama vya upinzani vilisusia uchaguzi lakini hakuna mabadiliko yoyote yaliyotokea. Hivyo kususia uchaguzi si jawabu" alisema Kabwe

Tanzania inaelekea katika uchaguzi mkuu mnamo mwezi Oktoba mwaka huu. Tayari chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekwisha teuwa wagombea wake wa urais kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Julai 6, mwaka huu bwana Membe alirejesha kadi ya uanachama wa Chama cha CCM.

Kiongozi huyo wa zamani alirudisha kadi ya uanachama ingawa Chama cha Mapinduzi kilishamfukuza uanachama .

Membe alidai kuwa taratibu za kichama hazikufuatwa, na hivyo bado alikuwa mwanachama halali wa CCM.

Tuhuma dhidi ya Membe ndani ya CCM

Membe alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kukiuka maadili pamoja na viongozi wengine waandamizi wawili makatibu wakuu wa zamani Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana, ambao wao hawajafukuzwa.

Katibu Mwenezi wa CCM Humphrey Polepole alidai kuwa mwenendo wa Membe ulikuwa si wa kuridhisha toka mwaka 2014.

"Kamati Kuu imeazimia kwa kauli moja kwamba Bernard Membe afukuzwe uanachama wa CCM. Uamuzi huu umekuja baada ya kuwa taarifa zake ndani ya chama zinaonesha mwenendo wake kutoka mwaka 2014 ambako katika chama amewahi kupata adhabu nyingine ambazo zingeweza kumsaidia kujirekebisha," alieleza Polepole.

Madai ya hujuma

Membe alikuwa akituhumiwa na baadhi ya wanachama wa chama hicho kuwa anajipanga 'kumhujumu' Magufuli katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Membe alikuwa akihusishwa kwa muda mrefu na mipango ya kutaka kugombea tiketi ya urais kupitia CCM mwaka huu, hatua ambayo baadhi waliitafsiri kama usaliti.

Japo katiba ya CCM inaruhusu hilo, imekuwa ni ada ya chama kumuachia rais aliye madarakani kupita bila kupingwa kwa awamu ya pili ya urais