Waziri wa Ulinzi wa Tanzania Dkt Hussein Mwinyi amepitishwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya chama cha CCM kugombea urais wa ZanzibarCHANZO CHA PICHA,TWITTER
Maelezo ya picha,
Waziri wa Ulinzi wa Tanzania Dkt Hussein Mwinyi amepitishwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya chama cha CCM kugombea urais wa Zanzibar
Waziri wa Ulinzi wa Tanzania Dkt Hussein Mwinyi amepitishwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya chama cha CCM kugombea urais wa Zanzibar.
Ni Mbunge wa jimbo la Kwahani, Zanzibar na Waziri wa Ulinzi katika serikali ya muungano. Huyu ni mtoto wa Rais mstaafu wa awamu ya pili ya serikali ya Jamhuri ya Mungaano wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Jina la Mwinyi sasa litapelekwa kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ili kumthibitisha rasmi kuwa mgombea wa CCM Zanzibar.
Dkt Mwinyi amepitishwa kwa kura 129 sawa na asilimia 78 ya kura zote.
Mwinyi alikuwa akikabiliana na upinzani kutoka kwa wanachama wenzake akiwemo Shamsi Vua Nahodha aliyepata kura 16 na Dkt Khalid Salim Mohammed aliyepata kura 19.
Baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa kura hizo Mwinyi aliwashukuru wajumbe wote kwa kuonesha imani kwake.
"Hizi ni kura nyingi sana...nikuahidini kuwa tutakuwa pamoja tukatafute ushindi wa Chama Cha Mapinduzi,"
Je ni kweli rais wa Zanzibar 'hupangwa' Dodoma?
Ni nani wanaopigiwa hesabu kuwania tiketi ya urais Zanzibar kupitia CCM?
Katika nyakati hizi zenye vijana wengi wanao hoji mara kwa mara maslahi ya Zanzibar katika Muungano na Tanganyika, Dkt. Mwinyi ambaye ni tabibu kitaaluma, anaonekana kuwa kichwa muhimu kuipeperusha bendera ya CCM Zanzibar, si kwa sababu tu ya siasa zake za utiifu, pia ni kwakuwa uhusiano wake kisiasa na kidamu uko pande zote mbili za muungano.
Yuko katika shughuli za kisiasa tangu mwaka 2000, hapa ni kusema sio mgeni katika uwanda wa siasa za Tanzania.
Ametumikia nafasi ya ubunge pande zote za Muungano, alikuwa Mbunge katika jimbo la Mkuranga, mkoa wa Pwani kabla ya kuwa Mbunge wa Kwahani.
Hii ina maana safari yake ya kisiasa inafanana na ya baba yake aliyetumikia nafasi ya urais pande zote za Muungano.
Rais wa sasa Dkt. Ali Mohamed Shein anamaliza miaka yake kumi ya kuiongoza Zanzibar, nchi ya visiwa na yenye mamlaka ya ndani pekee.
0 Comments