Iran imesema kwamba imemnyonga aliyekuwa afisa wake wa wizara ya ulinzi ambaye alipatikana na hatia ya kuuzia Marekani taarifa za makombora yake.
Afisa huyo Reza Asgari alinyongwa wiki iliyopita, kwa mujibu wa msemaji wa mahakama Gholamhossein Esmaili.
Bwana Esmaili alisema kwamba Asgari alikuwa ametoa taarifa kuhusu mpango wa makombora wa Iran kwa Shirika la Ujasusi la Marekani baada ya kustaafu kutoka wizara ya ulinzi kitengo cha angani 2016.
Hakusema Asgari alikamatwa lini, akashtakiwa lini au kufungwa kwake.
Bwana Esmaili alitangaza hilo wakati anajibu swali kuhusu kuhukumiwa kwa jasusi, Mahmoud Mousavi-Majd.
Alikuwa amehukumiwa kifo kwa kutoa taarifa za kijasusi kwa shirika la kijasusi la Marekani na shirika la kijasusi la Israel kuhusu mipangilio ya vikosi vya Iran nchini Syria.
Hakuna afisa wa Marekani aliyejibu moja kwa moja kuhusu hukumu iliyotolewa dhidi ya Asgari.
Julai mwaka jana, wizara ya Iran inayoshughulika na masuala ya ujasusi ilikamata watu 17 kwa makosa ya kukusanya taarifa za sekta ya nyuklia na kijeshi nchini humo kwa ajili ya kuzitoa kwa Shirika la Kijasusi la Marekani.
Wizara hiyo ilisema kwamba baadhi yao wamehukumiwa kifo lakini haikuwataja kwa majina.
Rais wa Marekani Donald Trump alitupilia mbali tangazo hilo na kulitaja kama "uongo mtupu".
Mwezi uliotangulia, aliyekuwa mkandarasi wa wizara ya ulinzi Iran, Jalal Hajizavar, alihukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya kutekeleza ujasusi.
Hajizavar inasemekana kwamba alikiri kuwa alilipwa ili kufanya upepelezi kwa ajili ya Shirika la Kijasusi la Marekani.
0 Comments