Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amesema kuwa "ameumizwa" na hatua ya Uturuki kugeuza Hekalu la Hagia Sophia mjini Istanbul kuwa msikiti.
Akizungumza katika ibada moja katika makao makuu ya Vatican, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki la Roma aliongeza kuwa mawazo yake "yapo na watu wa Istanbul".
Hagia Sophia ilijengwa kama hekalu la Wakristo karibu miaka 1,500 iliyopita na baadae kugeuzwa kuwa msikiti baada ya mapinduzi ya Ottoman ya mwaka 1453.
Hekalu hilo lililotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Unesco kama eneo la kihistoria duniani liligeuzwa kuwa makavazi ya kitaifa mwaka 1934 chini ya mwanzilishi wa nchi ya Uturuki padre Ataturk.
Lakini mapema wiki hii mahakama nchini Uturuki iliamuru kuondolewa kwa hadhi ya makavazi katika jengo hilo, ikisema matumizi yake mengine zaidi ya kuwa msikiti "haiwezekani kisheria".
Papa Francis alisema maneno machache kuhusu suala hilo: "Mawazo yangu yawafikie wakaazi wa Istanbul. Nifikiria kuhusu Santa Sophia nahisi uchungu sana."
Rais Recep Tayyip Erdogan amesema ibada ya kwanza ya Kiislamu itafanyika Hagia Sophia Julai 24.
Hekalu la Hagia Sophia lilikuwa na umuhimu mkubwa katika upande wa dini na siasa
Muda mfupi baada ya tangazo hilo, mwito wa kwanza wa sala au adhana ambayo ilipeperushwa katika vituo vyote vikuu vya habari ilisikika kutoka katika jengo hilo.
Vituo vya mitandao ya kijamii ya Hagia Sophia vimeondolewa mtandaoni.
Makundi yenye itikadi kali ya Kiislam nchini Uturuki kwa muda mrefu yamekuwa yakishinikiza eneo hilo ligeuzwe kuwa msikiti tena lakini wanazuoni na wanachama wa upinzani walipinga hatua hiyo.
Akitetea uamuzi huo, Rais Erdogan alisisitiza kuwa nchi yake imefikia uamuzi wa kitaifa ambao ni haki ya nchi inayojitawala, na kuongeza kuwa jengo hilo litakuwa wazi kwa watu wote- Waislamu, wasiokuwa Waislamu na wageni wa kimataifa.
'Maoni kutotiliwa maanani'
Papa ni mmoja wa viongozi kadhaa wa kidini na kisiasa duniani mbao wamekosoa hatua hiyo.
Baraza la Makanisa Duniani limetoa wito kwa Rais Erdogan kubatilisha uamuzi huo.
Kanisa la Urusi ambalo, lina idadi kubwa ya waumini wa Kikristo wa dhehebu la Orthodox duniani, moja kwa moja lilielezea kusikitishwa kwake na uamuzi uliotolewa a mahakama ya Uturuki likisema kuwa haikutilia maanani maoni yake kabla ya kuamua juu ya kuamua kuhusu kesi ya Hagia Sophia.
Hekalu hilo lilikuwa kivutio kikubwa cha watalii
Hatua hiyo pia imekosolewa vikali na Ugiriki huku Unesco ikisema Kamati ya Kimataifa kuhusu maeneo ya Kihistoria Duniani huenda ikatathmini upya hadhi ya eneo hilo la kale.
Mmoja wa waandishi maarufu wa Uturuki, Orhan Pamuk, ameiambia BBC kuwa hatua hiyo huenda ikaondoa "fahari" waliokuwa nayo Waturuki dhidi ya nchi hiyo ya Kiislam.
"Kuna mamilioni ya Waturuki kama mimi ambao walipinga hatua hii na ambao sauti zao hazikusikika," alisema Bw. Pamuk.
0 Comments