Charles Bukeko maarufu kama 'Papa Shirandula' aliaga dunia katika hospitali ya Karen mjini Nairobi

Mwigizaji maarufu wa Kenya Charles Bukeko, maarufu Papa Shirandula, ''alifariki akisubiri kupokea matibabu'' katika hospitali moja jijini Nairobi, mjane wake amewaambia waombolezaji.

Bi Beatrice Ebbie Andega , alidokeza hayo Jumatatu Julai 20, wakati wa mazishi ya msanii huyo yaliyofanyika katika Kijiji chao cha Namisi-Bukeko eneo la Nanderema, Funyula kaunti ya Busia.

Shughuli nzima ya mazishi ilifanywa kuambatana na kanuni zilizowekwa na Wizara ya Afya nchini Kenya ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Mwili wa Papa Shirandula ulisalia kwenye gari la kubeba maiti baada ya kuwasili nyumbani kwao huku polisi na maafisa wa afya wakiulinda kwa karibu.

Aidha, inasemekana wenyeji walipewa taarifa za kutotangamana na waombolezaji waliotoka mji wa Nairobi.

Na punde tu magari yaliyobeba waombolezaji yalipowasili, yalinyunyiziwa dawa.

Gari la maiti

Wakati huohuo, baba yake, Cosmas Bukeko amekanusha madai ya kwamba mwigizaji huyo alikufa kwa ugonjwa wa virusi vya corona.

Amesema kuwa familia hiyo inahitaji maelezo zaidi kutoka hospitali kuhusu kile kilichotokea kijana wake alipoaga dunia.

"Kwa sasa ziwezi kusema chochote kuhusu ugonjwa wake hadi nitakapofanya mazungumzo na hospitali. Nitasafiri kurejea Nairobi na pamoja na mke wake, tutawasiliana na wakili kupata taarifa kamili kutoka hospitali," alisema.

Mbali na maafisa wa afya, polisi na familia kidogo ya karibu waliokuwa nje, waombolezaji wengine walichungulia kupitia madirishani mwao wakati mwili unawasili nyumbani.

Mazishi ya Papa Shirandula

Bwana Bukeko aliyezaliwa 1963, alikuwa na kaka wanane na dada wanne.

"Alifanya mtihani wa kidato cha nne 1981 na kuajiriwa na serikali kama karani. Kisha akafanyakazi katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Chiromo kabla ya kuingia kwenye uigizaji," amesema Bwana Wafula.

"Kijana wangu amekuwa kila kitu kwetu. Alijenga nyumba zote katika hili boma. Yeye ndio ambaye amekuwa akisimamia kula kwetu. Hata hatujui umeme unalipwa pesa ngapi na hatujawahi kukatiwa hata siku moja," mama yake amesema.

Mwili wa Papa Shirandula umezikwa saa mbili na dakika 45 asubuhi baada ya ibada fupi ya kumuaga ambapo mke wake amedai kuwa Hospitali ya Karen ilizembea katika utenda kazi wake.

Punde tu baada ya mazishi watu waliombwa kutawanyika.