Hili ni taji la pili la La Liga Zidane akiwa mkufunzi wa Real Madrid

Zinedine Zidane anasema kwamba ushindi wa taji la kwanza na Real Madrid baada ya kipindi cha miaka mitatu umemfurahisha zaidi ya kushinda kombe la klabu bingwa Ulaya.

Real ilikamilisha ushindi huo huku ikiwa imesalia na mechi moja kucheza baada ya kuishinda Villareal katika uwanja wa Alfredo Di Stefano uliokuwa hauna mashabiki.

Karim Benzema alifunga kupitia shambulio lililopita katikati ya miguu ya kipa Sergio Asenjo na kuongeza bao la pili kupitia mkwaju wa penalti.

Katika tukio la kushangaza Sergio Amos alisaidia katika jaribio la kwanza ambapo Benzema alifunga lakini juhudi hiyo ikakataliwa.

Vicente Iborra aliipatia timu yake bao la kufutia machozi ambalo halikubadili ushindi wa Real Madrid wa 34 wa taji la Uhispania.

Timu hiyo ya Zidane imeshinda mechi zote 10 ilizocheza tangu ligi ya Uhispania kuanza upya mwezi Juni.

Wachezaji wa Real Madrid wakifurahia ushindi wao wa taji la La liga

Wanaingia katika mechi yao ya mwisho wakiwa na uongozi wa pointi saba mbele ya Bareclona waliopo katika nafasi ya pili.

''Hii ni bora zaidi ya chochote kile. Inachukua juhudi kubwa kushinda La Liga'', alisema mkufunzi huyo wa Real Madrid.

''Baada ya dakika 38 una pointi nyingi zaidi ya timu nyengine yoyote . Baada ya masharti ya kutotoka nje na kila kitu, ni kitu cha kufurahisha kwa kweli''.